Show abstract

UTAMBULISHO WA JINSIA KATIKA MAUMBILE SI HUJA NA PARADISO

Lengo la utafiti huu limekuwa ni kuchunguza na kuchanganua utambulisho wa jinsia katika kazi za John Habwe za Maumbile si Huja na Paradiso. Mada hii imechaguliwa kutokana na uelewa kuwa kazi za kifasihi huibua utambulisho wa jinsia tofauti. Dira ambayo imetuongoza kufanya utafiti huu ni nadharia ya Ufeministi wa Kiafrika. Tumechagua nadharia hii kuchunguza na kuchanganua utambulisho wa jinsia kwa kuchunguza uhusiano wao katika mazingira ya Kiafrika kwa kuwa imeandikwa kwa msingi wa Kiafrika. Nadharia hii huonyesha jinsi asasi za jamii za Kiafrika huchangia katika dhuluma za kijinsia. Pia, nadharia hii hutoa mapendekezo ya namna ya kupigania ukombozi, usawa na haki ya jinsia katika jamii. Malengo ambayo tumeshughulikia ni kubainisha jinsi asasi za jamii kupitia tamaduni zake zinavyoathiri mazingira ya utambulisho wa jinsia, kuangazia namna jinsia za kike na kiume zinavyoathirika kutokana na changamoto zinazopitia katika harakati za kutaka kujitambua na kutambulishwa na kudhihirisha mabadiliko ya mielekeo ya jamii kupitia fasihi kama nyenzo muhimu inayochangia mabadiliko hayo. Mbinu ambayo tumetumia katika utafiti huu ni ile ya kukusanya matini za data ya utafiti kutoka vitabuni maktabani. Matokeo ya utafiti wetu ni kuwa, asasi za jamii kama vile, ndoa, dini, utamaduni, uchumi, siasa na uongozi huchangia dhuluma za jinsia. Aidha, tumeona kuwa kuna njia anuwai zinazoweza kutumiwa kuleta ukombozi na usawa wa jinsia. Vile vile, tumegundua kuwa harakati za jinsia kutaka kujitambua na kutambuliwa na jamii zinachangia mabadiliko katika mielekeo ya jamii kutokana na mabadiliko katika majukumu ya jinsia kama yanavyowekewa msingi na utamaduni wa Kiafrika.

more details

Author: atieno jacqueline
Contributed by: olivia rose
Institution: university of nairobi
Level: university
Sublevel: post-graduate
Type: dissertations