Show abstract

MTINDO KATIKA UTENZI WA VITA VYA UHUD

Tasnifu hii inahusu uhakiki wa kimtindo wa Utenzi wa Vita vya Uhud nakala ya Haji Chum 1970. Tumehakiki namna vipengele vya kimtindo vimetumika katika utenzi huu kama vile: wahusika na uhusika wao, muundo, tamathali za usemi, mbinu rejeshi, taswira, mandhari na usimulizi. Nadharia ya umtindo imetufaa katika kuhakiki namna vipengele hivyo vimetumika kuufanikisha utenzi wetu. Katika utafiti wetu tumeongozwa na malengo matatu ambayo ni pamoja na kubainisha vipengele vya kimtindo vinavyotumika katika utenzi huu, pili tumechunguza nafasi ya vipengele hivyo katika kufanikisha utenzi wetu na mwisho tumebainisha namna muundo umejitokeza katika Utenzi wa Vita vya Uhud. Tumehakiki sifa za wahusika zinazowatambulisha na uhusika wao katika utenzi huu. Tumegundua kuwa tamathali za usemi zimetumika kumsaidia msanii kuwasilisha dhamira na maudhui ya utenzi huu. Vile vile, katika utenzi huu kuna mandhari ya kivita, kidini na kijiografia ambamo utenzi wenyewe umefumbatwa. Muundo wa utenzi huu pia umejitokeza wazi wazi pamoja na aina tatu za usimulizi zimeangaziwa. Maswali yetu ya utafiti yamepata majibu kikamilifu kwani tumeweza kubainisha wazi vipengele vya kimtindo ambavyo vimetumika katika utenzi huu na kubainisha nafasi zao. Tumefafanua changamoto tulizopitia na kuelezea namna tulivyozisuluhisha. Mwisho tumetoa mapendekezo kwa watafiti wa baadaye kuhusiana na Utenzi wa Vita vya Uhud.

more details

Author: obwogi, dickens, b
Contributed by: zemuhindi
Institution: university of nairobi
Level: university
Sublevel: post-graduate
Type: dissertations