Show abstract
ATHARI ZA SHENG’ KWA KISWAHILI MIONGONI MWA WATACHONI WAISHIO LWANDETI.
Tasnifu hii imeshughulikia utafiti kuhusu athari za lugha kipindi ya Sheng’ miongoni mwa wanafunzi wa Kiswahili ambao ni wazaliwa Watachoni na wanaotoka katika lokesheni ya Lwandeti. Tumetalii vyanzo vya utumizi wa lugha hii ya Sheng’ kwa kuangalia ni kwa namna gani leksimu za Sheng’ huundwa na ni kwa kiwango gani lugha hii imeathiri lugha sanifu ya Kiswahili haswa katika kitengo cha kimofolojia na kile cha kisemantiki. Pia tumeangalia ni kwa namna gani makosa haya yatokanayo na Sheng’ huathiri wanafunzi katika shule za upili ambazo ni pamoja na shule ya upili ya Lukhokho, shule ya upili ya Lwandeti D.E.B na shule ya upili ya Maturu katika kiwango cha mitihani ambayo ni ya kitaifa. Tumetumia mifano ya Insha ambazo wanafunzi hawa wameziandika kisha kuonyesha makosa ambayo wamefanya kwa kupigia mistari makosa hayo na kisha kuonyesha majibu sahihi juu yake kwa kutumia kalamu ya wino mwekundu. Pia, tumehoji walimu wanaolifunza somo hili la Kiswahili na kutambua jinsi lugha hii huenea katika mazingira ya shuleni. Vijana wengi haswa wa mijini wanatumia lugha hii ya Sheng’ katika mawasiliano yao hivyo utafiti huu umeonyesha kwamba siyo tu vijana wa mijini wanaoitumia lugha hii bali pia imeenea vijijini na kutumika na vijana wote katika mawasiliano yao. Tumependekeza tafiti zaidi zifanywe kuhusiana na suala hili nyeti ili kuepusha athari hasi kama hizi sio tu miongoni mwa wanafunzi wa Kiswahili walio Watachoni bali wakenya kwa jumla.
more details
- download pdf
- 0 of 0
- 150%